Wednesday, April 05, 2006

KASI MPYA SAWA LAKINI MMMHHH!

Mvuto wa watanzania kuhusu falsafa ya awamu ya nne ya uongozi wa nchi hususani kiongozi mkuu wa awamu hiyo unaweza ukawaingia nyongo watanzania kama si kuwatokea puani kama kasi hiyo haitakuwa na mwelekeo.

Awamu ya nne imeingia madarakani kwa kasi, Ari na Nguvu mpya kweli kama inavyojinadi yenyewe lakini kwa uapnde wangu naiona kasi hiyo hiyo inaelekea nisipokujua ndio maana napatwa na wasiwasi na kasi hiyo.

Watanzania wanyonge walio wengi kwa muda sasa wamekuwa watu wasio na matumaini wala uhakiak wa maisha yao ya kesho. Wengi wakiishi katika ufukara uliopitiliza bila shaka mkuu wa Kasi mpya analijua hilo ndio maana ya kauli mbiu yake maisha bora kwa kila Mtanzania.

Matumaini ya watanzania kwa awamu ya nne yamekuwa kuitegemea kasi hiyo kuwatoa walipo na kuwafikisha mahala fulani. Bila shaka katika hali nzuri kuliko waliokuwa nayo awali. Sasa tena kama Kasi mpya itawapeleka kwa nguvu na ari mpya katika hali mbaya zaidi ya hapo walipokuwa nachelea kusema yatatokea mengine ambayo binafsi yangu nisingependa hata kuyafikiria.

Kasi mpya inapoanza na kusema kuwa Bwawa la Mtera halitafungwa bila hata kujua majaliwa ya mvua na bila kuzingatia maelekezo ya kitaalamu hii kasi inatisha.

Ari mpya inapotumika kuwaondoa wafanya biashara ndogondogo na wapiga debe kwa lengo la kusafisha jiji bila kuandaa mipango mahsusi kwa ajili yao na bila kujiuliza kulikoni tumezalisha jeshi kubwa la ‘wala unga’ ambao wameamua kujiajiri kwa kutumia sauti zao vituoni huku wakichomoa na kufanya rabsha za hapa na pale kadri ya ulevi wanaotumia utakavyowatuma hii ni ari mpya ya mlevi.

Nguvu mpya inayotumika katika kuyatunza mazingira na kuwanyang’anya mazingira kwa kumnyanga’anya mnyonge kile anachokitegemea kwa mlo wake duni wa siku bila mkakati wowote wa maana wa kumfanya aendelee kuishi hii ni nguvu ya unyanganyi, udhulumati na ukatili kupindukia. Utunzaji wa mazingira ni lazima uwe stahimilivu (sustainable) kwa maana mazingira yanayotunzwa ni lazima pia yamtunze huyo binadamu kwa kumpatia mahitaji yake muhimu. Kutunza mazingira tu bila kujali maisha ya binadamu huo ni uwendawazimu.

Mama mchimba kokoto wa kule Wazo ambaye kuponda kokoto ndiko kulikokuwa njia yake pakee ya kujikomboa na umasikini leo ameachwa ‘uchi’ akiadhirika. Mlo wake na wa familia yake sasa ni mtihani wa chuo kikuu wakati yeye hata darasa la saba hajawahi kulikanyaga. Ada ya kusomeshea watoto wake sasa ni kitendawili, anachimbiwa kaburi yeye na kizazi chake chote. Uwezekano wa kufa kwa njaa na maradhi yatokanayo na njaa ni mkubwa. Watoto wake kujitumbukiza katika shughuli za umalaya na uuzaji na utumiaji wa madawa ya kulevya ni vigumu kuepukika. Kitanda chake na godoro lake lipo hatarini kuchukuliwa na waliomkopesha, kama ni‘ FINCA’ au ‘ PRIDE’ sijui lakini godor litakwenda. Mkopo lazima urejeshwe hata kama unachomiliki hapa duniani ni pumzi tu.

Watanzania wauza mkaa na watumia mkaa hao ndio kiama chetu kimefika njia mbadala umeme kama hutaki hama nchi. Watanzania wanaoganga maisha yao ndani ya hifadhi za Taifa nao kitanzi chao chaja labda nao wajiguze kuwa wanyama njia mbadala yao sijaisikia.

Kasi mpya inamshughulikia vilivyo mnyonge huku nae akishangilia masikini ya mungu kwani tafakuri yake imekosa lishe nzuri hivyo uwezo wake wa kuchambua mambo kwa wepesi umebaki ‘ robo kibaba.’

Uwezo wa kufikiria miongoni mwetu umepungua ndio maana tunawaachia wachache wafanye maamuzi ya ovyo kwa niaba yetu. Wale wachache wanaojaribu kutuamsha na kuona yanayofanyika mbele yetu htuwaaungi mkono na hao wanaonekana vimbelembele na wanashughulikiwa ipasavyo wakati waovu wakiachwa wanadunda.

Hebu fikiri wale vijana madaktari waliokuwa wakidai madai yao ya haki kabisa ambayo hayahitaji elimu ya mzungu kuyajua walipoishia. Kuna wengine mpaka leo hii bado wanataabika kwa kudai haki yao ili wawe wafanisi katika kuyajali miasha ya watnzania. Haya niambie wabunge wao wamefanywa nini baada madai yao kuonekana ya kipuuzi wakati huu? Watanzania hatujui hilo? Tumefanya nini kuhakikisha vijana wetu japo walidhalauriwa basi wanatendewa haki . Tumefanya nini? Kasi mpya imefanya nini?

Wale wanyonge wa wazo wameadhibiwa je Baraza la Mazingira lenye Mwenyekiti asiye na umasikini wa fikra limefanywa nini? Halikuwapo siku zote hizo mpaka hali ikawa mbaya kiasi hicho? Mpaka Kasi mpya inaanzisha Kamati ya Mazingira ya Baraza la Mawaziri chombo maaulum cha kuokoa mazingira hili baraza lilikuwa wapi? Limetumia kiasi gani cha pesa walipa kodi masikini wa nchi hii kushughulika na suala moja tu la Karibu Textile miaka yote hiyo? Wahusika hawafai kuadhibiwa? Kasi mpya iko wapi kuwashughulikia hawa kwanza kabla ya wanyonge?

Kasi mpya hivi karibuni imefuta mitaala mipya katika elimu ya msingi na sekondari nchini. Mtaala uliofutwa kwa upande wa elimu ya msingi kwa upande mmoja ni ule ambao ulikuwa bado haujaanza kutumika rasmi kwani walimu waliopo hawakuwa na uwezo wa kuweza kuufundisha hivyo wakufunzi wakwa wanazunguka nchi nzima kuwafundisha walimu jinsi ya kuufundisha mtaala huo. Mitaala ilishafanyiwa kazi na kupitishwa an wizara ya elimu kwa gharama nyingi. Wataalamu wa mitaala wakaikubali, na sasa semina zinaendelea kuwafundisha walimu mara mitaala hiyo imefutwa na Kasi mpya kwa maslahi ya taifa. Wabunge wanashanglia kwa nguvu wakionyesha walikerwa na mtaala ambao ulikuwa utumike. Hapa ndio maana naseme tafakuri yetu ni robo kibaba. Hivi wabunge walikuwa hawajui kama kuna mtaala mpya? Kwani mabadiliko ya mtaala hayakupitia bungeni (Ingawa Bunge Jipya Wabunge karibu wote ni walewale)? Au pia Waziri wa wakati huo alipotoa tamko walilipuka kwa furaha nderemo na vifijo?

Haya sasa swali linakuja mtaala uliorejeshwa ni upi? Maana kwa mujibu wa vyombo vya habari (Mtanzania Toleo na 3619) mtaala uliofutwa ni ule uliobadilishwa mwaka 2004 na si kweli kwamba mtaala hou ndio uliyoyaunganisha masomo ya Jiografia , Historia na Uraia kuwa Maarifa ya Jamii. Somo la Maarifa ya Jamii lilikewepo toka katika mtaala wa mwaka 1996. Mtaala utakaofutwa sasa ni upi maana mabadiliko ya mtaala haya yalikuwa ya mara ya tatu. Swali lingine la kujiuliza je mtaala wetu wa vyuo vya ualimu ukoje? Uko tayari kwa mabadiloko hayo ya Kasi mpya ua kwa sababu tafakuri zetu hazifanyi kazi sawasawa tusijiulize hilo? Vipi wahusika ambao wameliingizia hasara Taifa kutokana na maamuzi hayo ambayo kwa mujibu wa Waziri Sitta hayakuzingatia maslahi ya Taifa? Kasi mpya itawaangalia tu huku ikiendelea kuwaadhibu walalahoi? Hebu fikiria ingekuwa ndio mwalimu wa shule ya msingi kafanya upotevu wa shilingi laki moja angekuwa wapi? Kasi mpya itawafanya nini wahusika? Kuwateua kuwa wabunge na baadae kuapa uwaziri? Je kama hilo lilikosewa mangapi mengine yalikosewa na Wizara ya Elimu? Vipi kuhusu HakiElimu? Serikali iliyopita iliapa kutoipa nafasi taasisi hiyo kwa kipindi kilichokuwa kimebaki cha Mtukufu Rais wa awaamu ya tatu. Nini msimamo wa Kasi mpya kuhusu hili?Kasi mpya isishughulike kuwalaghai wanyonge, Kasi mpya itumike kuwapa afueni wanyonge, kuwashughulikia wote walishiriki kuudhalilsha utanzania mpaka kuwafanya watu wasiokuwa na mamlaka juu ya maisha yao wenyewe.

Kasi mpya iwashughulikie waliokuwa viongozi na walio madarakani kwa sasa waliofuja mali na madaraka kwa kujikopesha hela za walalahoi pasi kuzilipa nakufanya maamuzi yanatoitia hasara taifa hili.

Kasi mpya iwashughulikie mabepari uchwara ambao wanawavuna watanzania wenzao na kuwaibiia huku wakijiafanya wanawapenda na kutaka kuwaendeleza. Hawa mabepari uchwara wamekosa fadhila kwani ni jasho la watanzania ndilo lililowafikisha hapo walipo. Hawa mabepari uchwara wameshiliki kufilisi mabenki na kushirikiana na watu wa nje kudhoofisha uchumi wetu. Kasi mpya iwashughulikie hawa kwanza. Isiwaonee aibu hata kama walijitokeza kufadhili kamati mbalimbali za uchaguzi ndani ya Chama.

Kasi mpya isiwe ya kukurupuka na kumpa Meya miezi mitatu asafishe jiji kasha akianza kazi Kasi mpya inasema haikueleweka na kutoa maamuzi tofauti. Kasi mpya ifanye maamuzi kwa kufanya utafiti wa kina si utashi wa watu wawili watatu.

Kuna madai ya nchi kuongozwa na wana mtandao na hayo madai hayajakanushwa Ili lisidharauliwe Kasi mpya ilijibu hili kuna mazingira yanayoweza kufanya hili liaminike hata kama halina ukweli wowote. Utamaduni huu wa kujibu madai yanayoelekezwa kwa Kasi mpya utaifanya Kasi mpya iheshimike zaidi na kujijengea uaminifu mbele ya wananchi wake. Kinyume chake sipendi yatokee yaliyomtokea waziri Mkuu aliyepita kwa kutojibu hoja nzito zenye kumuhusisha yeye mustakabali wa taifa matokeo leo anabakaki anatapatapa ‘too late.’

Mungu wabariki Watanzania
Zibariki Tafakuri Zetu