Thursday, January 26, 2006

boni na wenzako mnaoishi ughaibuni nawapa kiapande hicho kama kilivyoripotiwa na NIPASHE kuona hali jinsi ilivyo katika bongo yetuBaadhi ya Wabunge wamechachamaa na kuitaka serikali iwaongezee mishahara, posho na marupurupu ili kuwawezesha kuwatumikia wapiga kura wao kwa ufanisi zaidi. Lakini kwa upande mwingine wametaka madai hayo hayo yasiandikwe au kutangazwa katika vyombo vya habari, kwa maelezo kuwa zitachochea hisia mbaya na kuwafanya wasikubalike kwa wapiga kura wao. Wabunge hao walitoa mapendekezo hayo jana walipokuwa wakichangia mada kuhusu masharti ya Mbunge iliyotolewa na Katibu Mkuu Kiongozi, Bw. Philemon Luhanjo katika semina ya mafunzo inayoendelea jijini Dar es Salaam.

Hata hivyo, Bw. Luhanjo aliwaonya wabunge dhidi ya madai yao hayo na kuwataka wazingatie maslahi yanayokidhi matakwa ya usawa kwa wananchi wote katika kugawana pato la taifa linalotokana na vyanzo mbalimbali zikiwemo shughuli za uzalishaji mali zinazofanywa na wananchi. Alisema hatua ya kudai maslahi bora zaidi kuliko ya watumishi wengine, ni sawa na kuonyesha ubinafsi aliouita kuwa ’collective selfishness’.

Akichangia mada hiyo, Mbunge wa Sumbawanga Mjini, Bw. Paul Kimiti alisema madai yao yanatokana na ukweli kuwa wabunge wana majukumu mengi na makubwa ya kuwahudumia watu kuliko watumishi wengine wote. Bw. Kimiti aliwaonya wabunge wasilichukulie mzaha dai hilo wala kulionea aibu kwa kuwa ni miongoni mwa masuala nyeti yanayowahusu.

Mbunge huyo wa siku nyingi, alisema suala la kudai maslahi bora kwa wabunge liliwahi kufanyika pia mwaka 1980 ambapo Spika wa sasa, Bw. Samwel Sitta, Naibu Spika, Bi Anna Makinda na yeye (Kimiti) walikuwa miongoni mwa wabunge waliokuwa kwenye kundi la kudai maslahi hayo. Hata hivyo alisema madai hayo yalitoweka baada ya wajumbe kadhaa wa kundi hilo ’kutunukiwa’ Uwaziri katika serikali ya awamu ya pili. Bw. Kimiti alisema madai hayo ni muhimu kwa wabunge kwa vile Wakuu wa Mikoa wanapata kiasi kikubwa cha fedha kwa ajili ya shughuli za hamasa zenye mwelekeo wa kisiasa kwa wananchi.

Kwa mujibu wa Bw. Kimiti, hivi sasa wabunge wanapata mshahara wa Sh milioni 1.2 na kiasi kingine cha takribani Sh milioni moja kila mwezi kwa ajili ya kufanikisha huduma jimboni, fedha ambazo hazihusiani na posho na marupurupu mengine wanayoyapata kwenye vikao vya bunge, vikao vya mabaraza ya madiwani na wanapokuwa safarini.

Naye Naibu Waziri wa Elimu Bw. Ludovic Mwananzila alisema hatua ya wananchi kulalamika wakati wabunge wanapodai ongezeko hilo inatokana na uelewa wao mdogo walionao kuhusu wajibu wa Mbunge. Bw. Mwananzila alisema uelewa kama huo unachochewa na waandishi wa habari wanapoandika ama kutangaza habari zinazohusu madai ya ongezeko la maslahi ya wabunge, na hivyo kuwafanya (wabunge) wasikubalike kwa wapiga kura. Alisema kutokana na hali hiyo, habari zinazohusu madai ya wabunge kutaka ongezeko la mishahara, posho na marupurupu hazipaswi kuwafikia waandishi wa habari wala kutangazwa au kuandikwa kwenye vyombo vya habari.

Pia Bw. Mwananzila aliiomba serikali kutoa waraka maalum wenye lengo la kuwashawishi wananchi waamini kuwa posho za wabunge ni kwa ajili ya matumizi kama vile ya kununua mafuta ya magari yao na siyo vinginevyo. Naye Mbunge wa Iramba Mashariki, Bw. Mgana Msindai alisema alisema ongezeko hilo ni muhimu kwa vile litakuwa linakidhi mahitaji yao. Bw. Msindai aliyataja baadhi ya mahitaji hayo kuwa ni kulala kwenye hoteli zinazostahili wanapokuwa kwenye misafara ya Mawaziri wanaposafiri ndani ama nje ya nchi na kuwa na magari yenye hadhi isiyopungua Sh milioni 50.

Kwa upande wake, Mbunge wa Bahi Bw. William Kusila alisema wabunge ni hazina ya ufumbuzi wa matatizo ya wananchi hivyo wanapaswa kupata ongezeko la mishahara, posho na marupurupu. Katika kuchangia hoja hiyo, Bw. Kusila aliwahimiza wabunge wapya kuunga mkono madai ya kuongezewa posho, mishahara na marupurupu ili wamudu kuwahudumia wapiga kura wao vinginevyo wasitarajie kuchaguliwa tena. Bw. Kusila alisema watu wanaopinga hoja za madai ya ongezeko hilo wana kile alichokiita ’wivu wa jumla’ na kwamba hawana mapenzi mema na wabunge.

Naye Mbunge wa Rufiji, Profesa Idrissa Mtulia alisema wabunge na familia zao, wanastahili kutibiwa kwenye hospitali zenye hadhi ili kupata huduma mapema na hivyo kuwa na wakati mzuri wa kurejea kwa wapiga kura wao. Hata hivyo, mbali na kuwataka wafikirie kuhusu haki ya mgawanyo sawa wa pato la taifa, Bw. Luhanjo aliwahakikishia wabunge hao kuwa, pamoja na mambo mengine serikali itazifanyia kazi hoja zao.

10 Comments:

Blogger boniphace said...

Karibu Mustapha, nashangaa siku nyingi ulikuwa mbali na kufungua blogu yako. Nimefurahi kuwa umekuja na kuitikia wito. Nakimbia kwangu kukutangaza, pale sasa kuna marumbano ya ushairi kidogo lakini nitayaacha hayo ili nikupe fursa maana kazi hii uliyokuja nayo inaonyersha picha rasmi ya aina ya masuala ya kiuchunguzi na ya kujali raia yatakavyopewa kipaumbele katika Gazeti Tando lako. Karibu sana nimefurahi sasa tunaonana tena.

7:43 AM  
Blogger John Mwaipopo said...

Mustafa karibu ndugu yetu tushirikiane katika kubadilishana mawazo. Binadamu si wakamilifu na hivyo basi mijadala ya mtandaoni kama hivi inasaidia kunoa fikra na mitazamo yetu.

Karibu tena karibu

Mzee wa Baragumu

10:50 AM  
Blogger Martha Mtangoo said...

Ndugu yangu unajua kuwapa kura wabunge wa CCM yataka moyo sana? wananipa hasira sana kwa kudai maslahi afadhlai umpe kura mbunge wa CHADEMA ambaye angalau anajua akufanyia nini na kutimiza ahadi zake kwako kuliko hawa wa CCM wanajali maslahi yao kwa kujiamini kuwa lazima atarudi bungeni, sasa angalia huyo kimiti nimeanza kumsikia tangu nikiwa mdogo anataka kujenga ikulu yake naona na amesahau kilichompeleka bungeni anatakiwa kukumbshwa.

karibu sana kaka katika ulimwengu wa mablogist!! keep intouch cheers.

2:58 AM  
Blogger Ndesanjo Macha said...

Karibu sana Mustapha. Ni furaha ilioje.

2:35 PM  
Blogger Kaka Poli said...

Mimi na si-hasa samahani ni siasa ni majirani kweli. Lakini ujirani wetu ni wa mashaka kabisa. Huyu si-hasa anaendeshwa na viumbe fulani ambao wanaitwa wanasi-hasa, hawa jamaa mimi ndo siwaelewei hata kidogo ndugu yangu Mustapha [hivi wewe ni mwarabu au?]. Jamaa wanajaribu kuhakikisha kwanza mtaji waliouwekeza katika kutafuta huo utwawala wa majimbo na wa upendeleo unarudi kabla kitmtim hakija shika hatamu, maana bwana mkubwa JK amechimba mkwara mzito'ukichemsha anakutimua huku anakutazama usoni bila ya haya'. Sasa sisi wafa njaa huku Singida kwa mbunge wetu hiyo si issue kwake kwa wakati huu!!

Mnh karibu ndugu yangu Mustapha na changamoto zako chanya!!!

2:44 AM  
Blogger FOSEWERD Initiatives said...

hawa wabunge wanafaa kupigwa na maganda ya ndizi usoni! kuna bwana mmoja pale hotwire alishauri tutembelee tovuti ya bwana mmbunge andy love

http://www.andylovemp.com

nadhani kuna haja sasa ya wabunge wetu kuanzisha za kwao ili tuwafuatilie mienendo utendaji na uwezo wao!

kuna bwana mgine akasema hivi ni kwanini wakuu wa wilaya wasifanye kazi za kibunge? nikaona kama inalipa lipa vile! angalau kwa miaka mitano hivi kama Keenja alivyotengeneza dar.......

lakini pia kila kukicha nadhani kuna haja ya kuachana na mtindo tunaokwenda nao wa utawala wa kikoloni ila tuwe na serekali za majimbo, na moja ya serekali kuu..ni rahisi kubanana katika serekali za majimbo tofauti na mfumo wa sasa..kwa kweli katika sera za mbowe hii ni moja wapo ninaiaminia sana...

dada Mtangoo utamu wa ngoma ni hadi uicheze, na pia ukiumwa na nyoka basi hata unyasi utakustua..ni budi watu wapigwe na nyoka mguuni kwanza...watu wana uwezo tofauti kuchambua mabo na kuona mbele...huenda wewe ni uliyeona kwanza...nataka JK awabane kiasi kwamba ubunge uwe ni kazi ya kujitolea...watuachie wenyewe tuna moyo masaa manne kwenye blogu kila siku bila malipo!!!

karibu sana mustapha uwanja uko wazi!

8:07 AM  
Blogger Innocent Kasyate said...

Karibu bwana Mustapha,
Hayo ya wanasiasa mimi nafikiri hii ni fani ambayo ingeondolewa katika safu za utawala.
Kwa mfano hapa Uganda, wanasiasa ni afadhali huko TZ.Siasa imekuwa ni sehemu ya kutajirikia.Unajua ni kwa nini? Ni kwasababu uchumi wa nchi zetu umekwisha na ni kwenye siasa tu ndio watu wanaweza kutengeneza utajiri.
Nakwambia tumekwisha.

4:17 AM  
Blogger must said...

Suala la msingi ni kuwa tusikate tamaa. Rome haikujengwa siku moja. Mimi naona cha afadhali hakuna bwana Innocent. Hata huku tz wanasema bora Uganda na Kenya. Hawa wote ni mafisadi, umesikia Spika wa Bunge la Tanzania alivyowaambia wabunge eti mambo yametoka nje wananchi wamekasirika utamu umekwisha. Utamu gani anaouzungumzia hayawani yule? Kuna mtu anajiita IGP yeye alisema atauvalia njuga suala la ujambazi na taingia yeye mwenyewe kufanya doria. unajua tangu juzi ujambazi umezidi maradufu! sasa sijui kama anafanya doria au anafanya ujambazi?

5:33 AM  
Blogger Mikundu Matako Makalio Manundu said...

Poleni kwa kazi nzito za malumbano, mkitaka kupumzika kidogo basi mitie kwa Mzee wa Mikundu kujiliwaza, hakuna mjadala, malumbano wala siasa ni Mikundu tuu...kazi njema

http://mikundu.blogspot.com/

10:05 AM  
Blogger zarena kewat said...

That's what everyone likes. You have a good imagination. Great post thanks you
vimax canada

9:40 AM  

Post a Comment

<< Home