Wednesday, April 05, 2006

KASI MPYA SAWA LAKINI MMMHHH!

Mvuto wa watanzania kuhusu falsafa ya awamu ya nne ya uongozi wa nchi hususani kiongozi mkuu wa awamu hiyo unaweza ukawaingia nyongo watanzania kama si kuwatokea puani kama kasi hiyo haitakuwa na mwelekeo.

Awamu ya nne imeingia madarakani kwa kasi, Ari na Nguvu mpya kweli kama inavyojinadi yenyewe lakini kwa uapnde wangu naiona kasi hiyo hiyo inaelekea nisipokujua ndio maana napatwa na wasiwasi na kasi hiyo.

Watanzania wanyonge walio wengi kwa muda sasa wamekuwa watu wasio na matumaini wala uhakiak wa maisha yao ya kesho. Wengi wakiishi katika ufukara uliopitiliza bila shaka mkuu wa Kasi mpya analijua hilo ndio maana ya kauli mbiu yake maisha bora kwa kila Mtanzania.

Matumaini ya watanzania kwa awamu ya nne yamekuwa kuitegemea kasi hiyo kuwatoa walipo na kuwafikisha mahala fulani. Bila shaka katika hali nzuri kuliko waliokuwa nayo awali. Sasa tena kama Kasi mpya itawapeleka kwa nguvu na ari mpya katika hali mbaya zaidi ya hapo walipokuwa nachelea kusema yatatokea mengine ambayo binafsi yangu nisingependa hata kuyafikiria.

Kasi mpya inapoanza na kusema kuwa Bwawa la Mtera halitafungwa bila hata kujua majaliwa ya mvua na bila kuzingatia maelekezo ya kitaalamu hii kasi inatisha.

Ari mpya inapotumika kuwaondoa wafanya biashara ndogondogo na wapiga debe kwa lengo la kusafisha jiji bila kuandaa mipango mahsusi kwa ajili yao na bila kujiuliza kulikoni tumezalisha jeshi kubwa la ‘wala unga’ ambao wameamua kujiajiri kwa kutumia sauti zao vituoni huku wakichomoa na kufanya rabsha za hapa na pale kadri ya ulevi wanaotumia utakavyowatuma hii ni ari mpya ya mlevi.

Nguvu mpya inayotumika katika kuyatunza mazingira na kuwanyang’anya mazingira kwa kumnyanga’anya mnyonge kile anachokitegemea kwa mlo wake duni wa siku bila mkakati wowote wa maana wa kumfanya aendelee kuishi hii ni nguvu ya unyanganyi, udhulumati na ukatili kupindukia. Utunzaji wa mazingira ni lazima uwe stahimilivu (sustainable) kwa maana mazingira yanayotunzwa ni lazima pia yamtunze huyo binadamu kwa kumpatia mahitaji yake muhimu. Kutunza mazingira tu bila kujali maisha ya binadamu huo ni uwendawazimu.

Mama mchimba kokoto wa kule Wazo ambaye kuponda kokoto ndiko kulikokuwa njia yake pakee ya kujikomboa na umasikini leo ameachwa ‘uchi’ akiadhirika. Mlo wake na wa familia yake sasa ni mtihani wa chuo kikuu wakati yeye hata darasa la saba hajawahi kulikanyaga. Ada ya kusomeshea watoto wake sasa ni kitendawili, anachimbiwa kaburi yeye na kizazi chake chote. Uwezekano wa kufa kwa njaa na maradhi yatokanayo na njaa ni mkubwa. Watoto wake kujitumbukiza katika shughuli za umalaya na uuzaji na utumiaji wa madawa ya kulevya ni vigumu kuepukika. Kitanda chake na godoro lake lipo hatarini kuchukuliwa na waliomkopesha, kama ni‘ FINCA’ au ‘ PRIDE’ sijui lakini godor litakwenda. Mkopo lazima urejeshwe hata kama unachomiliki hapa duniani ni pumzi tu.

Watanzania wauza mkaa na watumia mkaa hao ndio kiama chetu kimefika njia mbadala umeme kama hutaki hama nchi. Watanzania wanaoganga maisha yao ndani ya hifadhi za Taifa nao kitanzi chao chaja labda nao wajiguze kuwa wanyama njia mbadala yao sijaisikia.

Kasi mpya inamshughulikia vilivyo mnyonge huku nae akishangilia masikini ya mungu kwani tafakuri yake imekosa lishe nzuri hivyo uwezo wake wa kuchambua mambo kwa wepesi umebaki ‘ robo kibaba.’

Uwezo wa kufikiria miongoni mwetu umepungua ndio maana tunawaachia wachache wafanye maamuzi ya ovyo kwa niaba yetu. Wale wachache wanaojaribu kutuamsha na kuona yanayofanyika mbele yetu htuwaaungi mkono na hao wanaonekana vimbelembele na wanashughulikiwa ipasavyo wakati waovu wakiachwa wanadunda.

Hebu fikiri wale vijana madaktari waliokuwa wakidai madai yao ya haki kabisa ambayo hayahitaji elimu ya mzungu kuyajua walipoishia. Kuna wengine mpaka leo hii bado wanataabika kwa kudai haki yao ili wawe wafanisi katika kuyajali miasha ya watnzania. Haya niambie wabunge wao wamefanywa nini baada madai yao kuonekana ya kipuuzi wakati huu? Watanzania hatujui hilo? Tumefanya nini kuhakikisha vijana wetu japo walidhalauriwa basi wanatendewa haki . Tumefanya nini? Kasi mpya imefanya nini?

Wale wanyonge wa wazo wameadhibiwa je Baraza la Mazingira lenye Mwenyekiti asiye na umasikini wa fikra limefanywa nini? Halikuwapo siku zote hizo mpaka hali ikawa mbaya kiasi hicho? Mpaka Kasi mpya inaanzisha Kamati ya Mazingira ya Baraza la Mawaziri chombo maaulum cha kuokoa mazingira hili baraza lilikuwa wapi? Limetumia kiasi gani cha pesa walipa kodi masikini wa nchi hii kushughulika na suala moja tu la Karibu Textile miaka yote hiyo? Wahusika hawafai kuadhibiwa? Kasi mpya iko wapi kuwashughulikia hawa kwanza kabla ya wanyonge?

Kasi mpya hivi karibuni imefuta mitaala mipya katika elimu ya msingi na sekondari nchini. Mtaala uliofutwa kwa upande wa elimu ya msingi kwa upande mmoja ni ule ambao ulikuwa bado haujaanza kutumika rasmi kwani walimu waliopo hawakuwa na uwezo wa kuweza kuufundisha hivyo wakufunzi wakwa wanazunguka nchi nzima kuwafundisha walimu jinsi ya kuufundisha mtaala huo. Mitaala ilishafanyiwa kazi na kupitishwa an wizara ya elimu kwa gharama nyingi. Wataalamu wa mitaala wakaikubali, na sasa semina zinaendelea kuwafundisha walimu mara mitaala hiyo imefutwa na Kasi mpya kwa maslahi ya taifa. Wabunge wanashanglia kwa nguvu wakionyesha walikerwa na mtaala ambao ulikuwa utumike. Hapa ndio maana naseme tafakuri yetu ni robo kibaba. Hivi wabunge walikuwa hawajui kama kuna mtaala mpya? Kwani mabadiliko ya mtaala hayakupitia bungeni (Ingawa Bunge Jipya Wabunge karibu wote ni walewale)? Au pia Waziri wa wakati huo alipotoa tamko walilipuka kwa furaha nderemo na vifijo?

Haya sasa swali linakuja mtaala uliorejeshwa ni upi? Maana kwa mujibu wa vyombo vya habari (Mtanzania Toleo na 3619) mtaala uliofutwa ni ule uliobadilishwa mwaka 2004 na si kweli kwamba mtaala hou ndio uliyoyaunganisha masomo ya Jiografia , Historia na Uraia kuwa Maarifa ya Jamii. Somo la Maarifa ya Jamii lilikewepo toka katika mtaala wa mwaka 1996. Mtaala utakaofutwa sasa ni upi maana mabadiliko ya mtaala haya yalikuwa ya mara ya tatu. Swali lingine la kujiuliza je mtaala wetu wa vyuo vya ualimu ukoje? Uko tayari kwa mabadiloko hayo ya Kasi mpya ua kwa sababu tafakuri zetu hazifanyi kazi sawasawa tusijiulize hilo? Vipi wahusika ambao wameliingizia hasara Taifa kutokana na maamuzi hayo ambayo kwa mujibu wa Waziri Sitta hayakuzingatia maslahi ya Taifa? Kasi mpya itawaangalia tu huku ikiendelea kuwaadhibu walalahoi? Hebu fikiria ingekuwa ndio mwalimu wa shule ya msingi kafanya upotevu wa shilingi laki moja angekuwa wapi? Kasi mpya itawafanya nini wahusika? Kuwateua kuwa wabunge na baadae kuapa uwaziri? Je kama hilo lilikosewa mangapi mengine yalikosewa na Wizara ya Elimu? Vipi kuhusu HakiElimu? Serikali iliyopita iliapa kutoipa nafasi taasisi hiyo kwa kipindi kilichokuwa kimebaki cha Mtukufu Rais wa awaamu ya tatu. Nini msimamo wa Kasi mpya kuhusu hili?Kasi mpya isishughulike kuwalaghai wanyonge, Kasi mpya itumike kuwapa afueni wanyonge, kuwashughulikia wote walishiriki kuudhalilsha utanzania mpaka kuwafanya watu wasiokuwa na mamlaka juu ya maisha yao wenyewe.

Kasi mpya iwashughulikie waliokuwa viongozi na walio madarakani kwa sasa waliofuja mali na madaraka kwa kujikopesha hela za walalahoi pasi kuzilipa nakufanya maamuzi yanatoitia hasara taifa hili.

Kasi mpya iwashughulikie mabepari uchwara ambao wanawavuna watanzania wenzao na kuwaibiia huku wakijiafanya wanawapenda na kutaka kuwaendeleza. Hawa mabepari uchwara wamekosa fadhila kwani ni jasho la watanzania ndilo lililowafikisha hapo walipo. Hawa mabepari uchwara wameshiliki kufilisi mabenki na kushirikiana na watu wa nje kudhoofisha uchumi wetu. Kasi mpya iwashughulikie hawa kwanza. Isiwaonee aibu hata kama walijitokeza kufadhili kamati mbalimbali za uchaguzi ndani ya Chama.

Kasi mpya isiwe ya kukurupuka na kumpa Meya miezi mitatu asafishe jiji kasha akianza kazi Kasi mpya inasema haikueleweka na kutoa maamuzi tofauti. Kasi mpya ifanye maamuzi kwa kufanya utafiti wa kina si utashi wa watu wawili watatu.

Kuna madai ya nchi kuongozwa na wana mtandao na hayo madai hayajakanushwa Ili lisidharauliwe Kasi mpya ilijibu hili kuna mazingira yanayoweza kufanya hili liaminike hata kama halina ukweli wowote. Utamaduni huu wa kujibu madai yanayoelekezwa kwa Kasi mpya utaifanya Kasi mpya iheshimike zaidi na kujijengea uaminifu mbele ya wananchi wake. Kinyume chake sipendi yatokee yaliyomtokea waziri Mkuu aliyepita kwa kutojibu hoja nzito zenye kumuhusisha yeye mustakabali wa taifa matokeo leo anabakaki anatapatapa ‘too late.’

Mungu wabariki Watanzania
Zibariki Tafakuri Zetu

Thursday, February 02, 2006

Waziri Mkuu Bw. Edward Lowassa, amewataka Watanzania kuiga mfamo wa Mwenyekiti Mtendaji wa IPP katika utunzaji na uhifadhi wa mazingira.

Bw. Lowassa amesema miti mingi iliyoko Mkoani Kilimanjaro imetokana na juhudi binafsi za Bw. Mengi. ’Nampongeza sana Bw. Mengi kwa juhudi zake kubwa za kupanda miti. Napenda wananchi wengi kuiga mfano huo’ alisema.

Hivi kumbe kupanda miti ndiko kutunza Mazingira? Mimi nilikuwa Sijui. Kwa hiyo hata kama mtu atakuwa na maelfu ya viwanda vinavyotoa gesi ya kuharibu ozoni atakuwa ametunza Mazingira. Nasikia ziwa Manyara limekauka kwa asilimia 95. Haya huyu Mwenyekiti wa kusimamia mazingira anayesifiwa na waziri Mkuu hakuwepo wakati hilo linaendelea kutokea? Kuna mtu ananinong'oneza hapa eti Uenyekiti wake wa mazingira ni wa kumshughulikia mmiliki wa Karibu Textile tu basi baada ya hapo ni kupozi tu mbele ya kamera
Haya niambieni wana globu Kenya hali kadhalika Tanzania, Malawi watu wanakufa na njaa kwa kukosa kula au kula majani na mizizi yenye sumu wakijaribu kujitibu kwa njaa.

Mama mmoja mwenye kiwanda cha kutengeneza chakula cha mbwa nchini New Zealand amejitolea kiasi kikubwa cha chakula cha mbwa anachotengeneza kwenda kuokoa maisha ya wananchi wa Kenya wanaokufa njaa.

serikali ya Kenya imekuja juu na kukasirishwa na kitendo hicho na imetoa tamko heri watoto wa Kenya kufa njaa kulikop kula chakula hicho.

Maswali yanakuja kuhusu ubora wa chakula hicho. Chakula kinadaiwa kuwa navirutubisho na bora hata kwa matumizi ya binadamu kwani mbwa wa Ulaya wanapewa hadhi kama binadamu na hata wengine wanachukuliwa kama wana familia.Hayo mimi nimesikia Siyajui kwani sijawahi fika Ulaya. Sasa basi chakula cha mbwa kinavyochukuliwa huku kwetu ni tofauti na ilivyo huko kwa wenzetu. Nawaomba wana mtandao mtoe maoni kuhusu hili, Je ni vema mtu kufa kuliko kula chakula cha mbwa? Je chakula tunachokiita cha binadamu huku kwetu kina tofauti yeyote na hicho chakula cha mbwa. Eti nasikia hata firigisi ambazo huku kwetu baba mwenye nyumba pekee ndiye anayeruhusiwa kula endapo kuku akichinjwa huko kwa wenzetu ni chakula nafuu cha mbwa? Eti hata ule unga wa njano tuliokuwa tukijichana miaka ya themanini kilikuwa chakula cha nguruwe?
Haya ndio mawazo ya spika la bunge la jamhuri ya muungano ya wadanganyika kuhusu ujinga wa wadnganyika kuwapokea tena maana vichwa vyao maji havikawii kusahau

Spika wa Bunge Bw. Samwel Sitta amewataka wabunge wasivunjike moyo kwa kufunikwa na wimbi zito la tuhuma zinahusiana na nyongeza ya maslahi yao. Bw. Sitta aliyasema hayo Jijini Dar es Salaam jana alipokuwa akifunga semina ya wiki mbili ya wabunge kuhusu kanuni na maadili katika Bunge. ’’Wabunge wapya mmsivunjike moyo kwa kufunikwa na wimbi la tuhuma, mzihesabu kama gharama za kuwa mwanasiasa,” alisema Spika huku akishangiliwa na wabunge.

Aliwataka wachukulie lawama hizo kama changamoto kwao wakiwa ni wanasiasa. Alisema wabunge wasitegemee kushangiliwa kila wakati na badala yake wajue kwamba kuna wakati watazomewa pia. Alisema mafanikio ya semina hiyo yametibuliwa kwa kiasi fulani na wimbi la lawama dhidi ya wabunge kuhusiana na mazungumzo katika mada ya masharti ya kazi ya mbunge iliyowasilishwa na Katibu Kiongozi Bw Philemon Luhanjo.

Alisema wachangiaji wa mada hiyo walieleza kwa uwazi mazingira ya utendaji wa kazi kwa wabunge na matatizo yanayowasibu katika kutekeleza wajibu wao. Alisema hata hivyo, michango ya wabunge juu ya maslahi yao imechukua kama dalili ya kutowajali wananchi.

Alisema hata ufafanuzi wake kuhusu suala hilo haukusaidia kuliweka jambo hilo sawa kwa sababu lilishajengewa mkondo ulioibua hisia mbaya katika jamii. ’’Sikukusudia hapa kutoa ufafanuzi mwingine juu ya maslahi ya wabunge katika mazingira haya ambayo hayaruhusu mjadala uliokamilifu,’’ alisema. ’’Kwa vyovyote vile masuala ya maslahi mbalimbali pamoja na wabunge kwa wakati hadi wakati yanaendelea kushughulikiwa na taasisi husika za Serikalini kwa mujibu wa taratibu zilizowekwa, aliongeza.

Pia aliwataka wabunge hao kutopoteza muda kufikiria kama wametendewa haki ama la. Alisema hautapita muda mrefu kwa wananchi kutambua kuwa waliowachagua ni wabunge safi na wazalendo. Alisema yeye ana imani kubwa na Bunge hilo na kuwa ni hazina ya kujivunia kwa uzoefu na taaluma mchanganyiko na kwamba lina dhamira ya dhati ya kutumikia taifa.

Monday, January 30, 2006

Hivi mnamkumbuka Reginald Mengi? Mtu ambaye kila siku anawaasa watanzania waondokane na umasikini wa fikra ili nao wawe tajiri kama yeye. Hivi mnafahamu jinsi wafanyakazi wake katika makampuni anazomoliki wanavyokuwa matajiri kwa sababu bosi wao anataka kuwa tajairi? mnafahamu jinsi anavyowapenda walemavu kiasi kwamba huwakaribisha kula nae chakula na kucheza nae Twanga pepeta? Mtu huyu safi eeeenh?
Mambo hayo! eti Supika wa bunge anadai kuwa wabunge wa Tanzania ndio wanaolipwa kidogo kuliko wote katika nchi za 'komoni " wealth. Sasa sijui anajua walimu wa tanzania, madaktari katika hiyo komoni wealth wanalipwaje? Ingekuwa vyema pia akajua ni kiasi gani watanzania tunakipata katika mikataba ya madini ikilinganishwa na nchi nyingine za komoni Weath, bei ya umeme je ikoje ukilinganisha na mahayo komoni weath. Halafu naomba nikumbusheni Eti Komoni wezi ndio kitu gani? na kinamuhusu vipi mpiga kura wa kule Igunga tabora?

Thursday, January 26, 2006

boni na wenzako mnaoishi ughaibuni nawapa kiapande hicho kama kilivyoripotiwa na NIPASHE kuona hali jinsi ilivyo katika bongo yetuBaadhi ya Wabunge wamechachamaa na kuitaka serikali iwaongezee mishahara, posho na marupurupu ili kuwawezesha kuwatumikia wapiga kura wao kwa ufanisi zaidi. Lakini kwa upande mwingine wametaka madai hayo hayo yasiandikwe au kutangazwa katika vyombo vya habari, kwa maelezo kuwa zitachochea hisia mbaya na kuwafanya wasikubalike kwa wapiga kura wao. Wabunge hao walitoa mapendekezo hayo jana walipokuwa wakichangia mada kuhusu masharti ya Mbunge iliyotolewa na Katibu Mkuu Kiongozi, Bw. Philemon Luhanjo katika semina ya mafunzo inayoendelea jijini Dar es Salaam.

Hata hivyo, Bw. Luhanjo aliwaonya wabunge dhidi ya madai yao hayo na kuwataka wazingatie maslahi yanayokidhi matakwa ya usawa kwa wananchi wote katika kugawana pato la taifa linalotokana na vyanzo mbalimbali zikiwemo shughuli za uzalishaji mali zinazofanywa na wananchi. Alisema hatua ya kudai maslahi bora zaidi kuliko ya watumishi wengine, ni sawa na kuonyesha ubinafsi aliouita kuwa ’collective selfishness’.

Akichangia mada hiyo, Mbunge wa Sumbawanga Mjini, Bw. Paul Kimiti alisema madai yao yanatokana na ukweli kuwa wabunge wana majukumu mengi na makubwa ya kuwahudumia watu kuliko watumishi wengine wote. Bw. Kimiti aliwaonya wabunge wasilichukulie mzaha dai hilo wala kulionea aibu kwa kuwa ni miongoni mwa masuala nyeti yanayowahusu.

Mbunge huyo wa siku nyingi, alisema suala la kudai maslahi bora kwa wabunge liliwahi kufanyika pia mwaka 1980 ambapo Spika wa sasa, Bw. Samwel Sitta, Naibu Spika, Bi Anna Makinda na yeye (Kimiti) walikuwa miongoni mwa wabunge waliokuwa kwenye kundi la kudai maslahi hayo. Hata hivyo alisema madai hayo yalitoweka baada ya wajumbe kadhaa wa kundi hilo ’kutunukiwa’ Uwaziri katika serikali ya awamu ya pili. Bw. Kimiti alisema madai hayo ni muhimu kwa wabunge kwa vile Wakuu wa Mikoa wanapata kiasi kikubwa cha fedha kwa ajili ya shughuli za hamasa zenye mwelekeo wa kisiasa kwa wananchi.

Kwa mujibu wa Bw. Kimiti, hivi sasa wabunge wanapata mshahara wa Sh milioni 1.2 na kiasi kingine cha takribani Sh milioni moja kila mwezi kwa ajili ya kufanikisha huduma jimboni, fedha ambazo hazihusiani na posho na marupurupu mengine wanayoyapata kwenye vikao vya bunge, vikao vya mabaraza ya madiwani na wanapokuwa safarini.

Naye Naibu Waziri wa Elimu Bw. Ludovic Mwananzila alisema hatua ya wananchi kulalamika wakati wabunge wanapodai ongezeko hilo inatokana na uelewa wao mdogo walionao kuhusu wajibu wa Mbunge. Bw. Mwananzila alisema uelewa kama huo unachochewa na waandishi wa habari wanapoandika ama kutangaza habari zinazohusu madai ya ongezeko la maslahi ya wabunge, na hivyo kuwafanya (wabunge) wasikubalike kwa wapiga kura. Alisema kutokana na hali hiyo, habari zinazohusu madai ya wabunge kutaka ongezeko la mishahara, posho na marupurupu hazipaswi kuwafikia waandishi wa habari wala kutangazwa au kuandikwa kwenye vyombo vya habari.

Pia Bw. Mwananzila aliiomba serikali kutoa waraka maalum wenye lengo la kuwashawishi wananchi waamini kuwa posho za wabunge ni kwa ajili ya matumizi kama vile ya kununua mafuta ya magari yao na siyo vinginevyo. Naye Mbunge wa Iramba Mashariki, Bw. Mgana Msindai alisema alisema ongezeko hilo ni muhimu kwa vile litakuwa linakidhi mahitaji yao. Bw. Msindai aliyataja baadhi ya mahitaji hayo kuwa ni kulala kwenye hoteli zinazostahili wanapokuwa kwenye misafara ya Mawaziri wanaposafiri ndani ama nje ya nchi na kuwa na magari yenye hadhi isiyopungua Sh milioni 50.

Kwa upande wake, Mbunge wa Bahi Bw. William Kusila alisema wabunge ni hazina ya ufumbuzi wa matatizo ya wananchi hivyo wanapaswa kupata ongezeko la mishahara, posho na marupurupu. Katika kuchangia hoja hiyo, Bw. Kusila aliwahimiza wabunge wapya kuunga mkono madai ya kuongezewa posho, mishahara na marupurupu ili wamudu kuwahudumia wapiga kura wao vinginevyo wasitarajie kuchaguliwa tena. Bw. Kusila alisema watu wanaopinga hoja za madai ya ongezeko hilo wana kile alichokiita ’wivu wa jumla’ na kwamba hawana mapenzi mema na wabunge.

Naye Mbunge wa Rufiji, Profesa Idrissa Mtulia alisema wabunge na familia zao, wanastahili kutibiwa kwenye hospitali zenye hadhi ili kupata huduma mapema na hivyo kuwa na wakati mzuri wa kurejea kwa wapiga kura wao. Hata hivyo, mbali na kuwataka wafikirie kuhusu haki ya mgawanyo sawa wa pato la taifa, Bw. Luhanjo aliwahakikishia wabunge hao kuwa, pamoja na mambo mengine serikali itazifanyia kazi hoja zao.